Taratibu za Kufanya Biashara ya Mazao ya Nyuki Ndani na Nje ya Nchi.
Utangulizi
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na utalii umepewa jukumu la kuhifadhi, kuendeleza, kusimamia rasilimali za nyuki ikiwemo biashara ya mazao ya nyuki.
Kwa mujibu wa sheria ya Ufugaji nyuki namba 242 ya mwaka 2002 sehemu ya 6 inatoa mamlaka ya kudhibiti, kufanya ukaguzi, kutoa leseni, kibali na cheti kwa wafanyabiashara wa mazao ya nyuki nchini. Aidha, kanuni za ufugaji nyuki za mwaka 2004 sehemu ya 37 – 54 inatoa taratibu za kufanya biashara ya mazao ya nyuki. Vilevile Tangazo la serikali Na 454 ya mwaka 2019 imeweka viwango vya tozo na biashara ya mazao ya nyuki na Huduma. Pia Mowngozo wa uhakiki wa ubora wa mazao ya nyuki wa mwaka 2007 unatoa maelekezo ya kufuata ili kulinda ubora na usalama wa asali.
Usajili
Sehemu ya 37 ya Kanuni za Ufugaji Nyuki inatamka wazi kuwa ni kosa kufanya biashara ya mazao ya nyuki bila kuwa na leseni. Utoaji wa leseni ni lazima ufanyike kwa kuzingatia sifa muhimu ambazo mwenye leseni atatakiwa kuwa nazo kwa kipindi chote leseni yake itakapo kuwa hai.
Maombi ya leseni au ya kurudia kuwa na leseni ni lazima yatumwe kwa Kamishna wa Uhifadhi kwenye ofisi za Mhifadhi Mkuu wa wilaya kwa kutumia fomu maalum na taratibu na ni lazima yaambatane na ada zilizoainishwa. Maombi ya kurudia kuwa na leseni ni lazima yafanyike siku 30 kabla ya kwisha kwa leseni.
Usajili umegawanyika katika sehemu kuu tatu:-
(i) Usajili kufanya biashara ndani ya nchi. (Apiary product dealers)
(ii) Usajili wa mkusanyaji wa mazao ya nyuki (Collection of apiary products)
(iii) Usajili kufanya biashara nje ya nchi.
Usajili wa kufanya biashara ndani ya nchi (Apiary Product Dealers)
Mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya mazao ya nyuki ndani ya nchi atatakiwa kuwa na nyaraka zifuatazo ili aweze kusajiliwa.
a) Jengo la kuchakata na kufungashia mazao ya nyuki lililosajiliwa
b) Nakala ya hati ya usajili wa jina la biashara au jina la kampuni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
c) Nakala ya Cheti cha mlipa kodi kutoka TRA pamoja na nambari ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN);
d) Kivuli cha kitambulisho (kitambulisho cha Utaifa, mpiga kura, leseni ya kundesha gari);
e) Muhtasari wa maelezo ya kampuni (MEMAT) kwa kampuni;
f) Leseni ya Biashara ya ndani kutoka kwa Afisa biashara wa wilaya.
g) Picha 3 za rangi (Passport Size);
h) Ada ya usajiri kwa mwaka wa serikali ambapo gharama yake ni shilingi 53,000= ( shilingi 3,000/= ni gharama ya fomu na 50,000/= ni Ada ya usajili)
Usajili wa mkusanyaji wa mazao ya nyuki (Collection of apiary products)
Mahitaji yote hapo juu isipokuwa (a)
Usajili wa kufanya biashara ya mazao ya nyuki nje ya nchi
Mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya mazao ya nyuki nje ya nchi atatakiwa kuwa na nyaraka zifuatazo ili aweze kusajiliwa: -
a) Jengo la kuchakatia mazao ya nyuki ambalo limekaguliwa na kuidhinishwa na shirika la viwango Tanzania (TBS) kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 13 cha taratibu za ufugaji nyuki. Endapo anapata huduma ya kuchakata mazao ya nyuki katika maeneo yanayotambulika naTFS atawasilisha nyaraka husika ya kumtambulisha.
b) Kivuli cha hati ya usajili wa biashara au jina la kampuni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA);
c) Kivuli cha hati ya mlipa kodi kutoka mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA);
d) Kivuli cha Kitambulisho (kitambulisho cha Utaifa, mpiga kura, au leseni ya kuendesha gari)
e) Muhtasari wa maelezo ya kampuni (kwa mtu mwenye kampuni).
f) Leseni ya Biashara ya ndani kutoka kwa Afisa Biashara.
g) Picha 3 za rangi (Passport Size).
h) Ada ya usajili kwa mwaka wa serikali ni shiling 110,000.00/= (10,000/= ni gharama ya fomu na 100,000/= ni Ada ya usajili).
Baada ya Mfanyabiashara wa mazao ya nyuki kupata usajili ili aweze kusafirisha mazao ya nyuki kwenda nje ya nchi atatakiwa kuwa kupata kibali cha kusafirisha mazao hayo ( export Permit)
Nyaraka muhimu ili kupata kibali cha kusafirisha mazao ya nyuki nje ya nchi ( export permit)
i. Mkataba wa mauzo (invoice) kutoka kwa mnunuzi utakaoonesha bei ya mazao kwa thamani ya dola za kimarekani au fedha zinazokubalika kimataifa, uzito au idadi ya mazao.
ii. Custom Declaration Form (TANSAD) kutoka mamlaka ya mapato (TRA).
iii. Taarifa ya matokeo ya uchambuzi wa sampuli ya mazao hasa asali kutoka kwenye maabara inayotambulika na Serikali.
NB. Kwa mujibu wa sheria ya Magonjwa ya Mifugo ya mwaka 2003 na Kanuni za udhibiti na usafirishaji wa mazao ya mifugo ya mwaka 2022, mtu yeyote anayesafirisha asali inayozidi kilo 15 (lita 10) kwenda nje ya nchi anapaswa kulipia shilingi 100,000/- na kila anayeingiza nchini asali zaidi ya kilo 15 (lita 10) anapaswa kulipia kiasi cha shilingi 200,000/- Fedha hizi zinalipwa kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo - Wizara ya Uvuvi na Mifugo
Hatua za kufuata na gharama za kufanya biashara ya mazao ya nyuki zinapatika katika tovuti ya Tantrade https://trade.tanzania.go.tz
Vibali/ Cheti
Mfanyabiashara atatakiwa kulipia gharama kabla ya kufanyiwa ukaguzi. Endapo mzigo husika hautakidhi vigezo /viwango cheti cha kusafirishia hakitatolewa na gharama za ada ya ukaguzi hazitarudishwa.
Hairuhusiwi kuweka lakiri kwenye mzigo kabla ya kukaguliwa endapo mfanyabiashara atakuwa ameweka lakiri kwenye mzigo husika cheti cha kusafirishia hakitatolewa.
Baada ya mfanyabiashara kukamilisha kulipia malipo stahili ya mzigo wake,atapewa vibali vifuatavyo:
i. Kibali cha kusafirishia mzigo nje ya nchi.
ii. Cheti cha usafi cha asali au nta.
iii. Cheti cha usafi cha jumuiya ya umoja wa Ulaya endapo atakuwa anapeleka kwenye soko ulaya.
Usafirishaji ndani ya nchi
i. Wafanyabiashara wanaosafirisha mazao ya nyuki (asali, nta ) ndani ya nchi kutoka wilaya moja hadi nyingine au mkoa mmoja kwenda mwingine watatakiwa kuwa na hati ya kusafiria “Transit Pass (TP)” pamoja na risiti ya ushuru katoka wilaya husika. Ushuru wa halmashauri huwekwa kwa mujibu wa sheria ndogo na hutofautiana kati ya wilaya moja na nyingine
ii. Wafanyabiashara watatakiwa kufuata muongozo wa udhibiti wa ubora ili kuwa na asali inayokidhi viwango. Hataruhusiwa mfanyabiashara/mfugaji yeyote kusafirisha asali iliyofungashwa kwenye vyombo vilivyokwisha kutumika kuhifadhi bidhaa zingine kama vile sabuni, dizeli, mafuta nk.
iii. Endapo atapatikana mtu yeyote atakayekiuka taratibu hizo mzigo utazuiwa na mhusika atatozwa faini kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ufugaji Nyuki Na.15 ya mwaka 2002.
Hitimisho
Ubora wa mazao ya nyuki ni muhimu kuzingatiwa kwa kuwa asali ni chakula, hivyo tuepuka kuchafua asali kwa lengo la kutaka kupata faida na pia tumia vifungashio sahihi ili kutuza ubora .